Katika kikao cha Bunge la Taifa Jumamosi, Khwaja Asif, Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, amesema kuwa Iran na Pakistan zina uhusiano wa kihistoria wa karne nyingi, na kwamba “Islamabad itasimama bega kwa bega na Iran na itaendelea kuwatetea katika kila jukwaa la kimataifa ili kulinda maslahi ya Iran.”
Akitaka kuwepo mshikamano wa Kiislamu, Asif amehimiza Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuitisha mkutano wa dharura mara moja na kuandaa mkakati wa pamoja wa kukabiliana na uchokozi wa Israel.
Ameonya kuwa ulimwengu wa Kiislamu ni lazima uchukue hatua sasa, la sivyo utakumbwa na mashambulizi kama yale yanayoikumba Iran.
"Israel imeshambulia Iran, Yemen, na Palestina," amesisitiza. "Ikiwa mataifa ya Kiislamu hayataungana sasa, kila moja litaonja madhara ya mashambulizi hayo kwa wakati wake."
Asif pia amegusia maandamano yanayoongezeka katika mataifa ya Magharibi dhidi ya Israel, akisema kuwa hata watu wasio Waislamu wameamka dhamira, wakati ulimwengu wa Kiislamu unaendelea kuwa kimya.
"Dhamira yao imeamka, tofauti na ulimwengu wa Kiislamu," amesema kwa masikitiko.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Ishaq Dar, siku ya Ijumaa alilaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran, akiyataja kuwa ni "ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya Iran," na kuonesha mshikamano na serikali na wananchi wa Iran.
Dar pia alitoa rambirambi zake za dhati kufuatia vifo vya raia wengi katika mashambulizi hayo ya Israel.
Kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alilaani vikali mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Iran kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii X.
"Ninalaani kwa maneno makali zaidi mashambulizi ya kichokozi ya Israel dhidi ya Iran," aliandika. "Nawasilisha rambirambi zangu za dhati kwa wananchi wa Iran kwa kupoteza maisha katika shambulio hili. Hatua hii ya kikatili na isiyo ya uwajibikaji wowote ni ya kutisha na inatishia kuuchafua zaidi ukanda ambao tayari uko kwenye hali tete. Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka ili kuzuia kuongezeka kwa hali hii ambayo inaweza kuhatarisha amani ya kikanda na ya dunia kwa ujumla," aliongeza.
Wakati huohuo, Rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari, katika taarifa yake ya Ijumaa, alilaani vikali mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya Iran.
"Mashambulizi haya ni uvunjaji mkubwa wa mamlaka ya kitaifa na ukamilifu wa ardhi ya Iran, na yanaonesha dharau kamili kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na misingi ya sheria za kimataifa," alisema Zardari.
Rais huyo pia alieleza masikitiko yake ya dhati kwa watu wa Iran kutokana na vifo vya raia waliopoteza maisha kutokana na mashambulizi hayo, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka kumwajibisha mhalifu na kuzuia hali hiyo isizidi kuwa mbaya zaidi.
342/
Your Comment